Saturday, March 5, 2016

Aina za Kuku

Mtu anapotaka kuanza ufugaji wa kuku anaweza kuwa anajiuliza afuge kuku wa aina kwa sababu kuna aina tofauti za kuku. Leo tutaelezea aina ambazo hufugwa mara nyingi hapa Tanzania na kuzichambua kidogo ili kumpa mwanga mfugaji kuamua afuge aina ipi na hata mlaji kuamua ale nyama ipi.
  1. Kuku wa kisasa: Hawa ni kuku ambao kosaafu (breed) yao imetengenezwa nje ya Tanzania. Mara nyingi huwa kuku wazazi wa hawa kuku wa kisasa huwa wanaingizwa nchini kutoka Uholanzi, Uingereza au Marekani. Hawa kuku wazazi ni kuku maalum ambao kazi kubwa imefanyika kutengeneza kosaafu yake. Kosaafu hizi hutengenezwa na wataalam wa hali ya juu ndio maana kuku hawa wana tabia tofauti na wale wa kienyeji; wale wa nyama wanakua haraka sana na wa mayai wanataga zaidi ya wale wa kienyeji. Lakini kuku wa kisasa wana uwezo mdogo wa kustahimili magonjwa na ladha ya nyama na mayai yake sio nzuri kama ile ya kuku wa kienyeji. Kama ambavyo nimegusia, kuku wa kizungu wapo wa nyama (broilers) na wa mayai (layers). Kuku wa nyama hufugwa kwa kulishwa chakula maalum na kuwa tayari kuuzwa baada ya wiki sita hadi nane. Bei yake sokoni ni kati ya Tshs 5000-7000. Kuku wa mayai wao huanza kutaga takribani wiki ya 20 na hendelea kutaga hadi wiki ya 80 kama watakuwa wametunza inavyotakiwa. Trei moja la mayai huuzwa kwa Tshs 7000-10000 kulingana na upatikanaji wake kwa wakati huo.
  2. Chotara: Hawa ni kuku mchanganyiko wa kisasa na kienyeji. Wanapatikana kutoka kwa kuku jike wa kienyeji na dume wa kisasa. Chotara wao huwa na tabia za kuku wa kienyeji na kisasa. Wanachukua tabia za kuku wa kisasa kwenye uzito na ukuaji. Chotara huwa wakubwa na ukuaji wake ni wa haraka ukilinganisha na wa kuku wa kienyeji. Pia wanachukua tabia ya kuku wa kienyeji kwenye ustahimilivu wa magonjwa, ladha ya nyama na mayai na uwezo wa kuatamia. Kuku hawa humuhakikishia mfugaji faida ya haraka. Bei yake sokoni ni kuanzia Tshs 10,000 kulingana na ukubwa wa kuku na mayai trei Tshs 12,000-15,000.
  3. Kuku wa kienyeji: Hawa ni kuku wenye asili ya hapa kwetu Tanzania mfano mzuri na kuku maarufu wa singida waitwao Kuchi. Kuku hawa wanapendwa zaidi kwa sababu ya ladha ya nyama yake na mayai. Na wananauwezo mkubwa wa kustahimili magonjwa, kujitafutia chakula na kuatamia. lakini mara nyingi kuku hawa wana miili midogo na hawatagi kwa wingi sana. Hata hivyo biashara ya kuku wa kienyeji ni nzuri kwa sababu wanapatikana kwa nadra sana. Bei ya kuku na mayai ya kienyeji ni kama ile ya chotara.
Biashara ya kuku kwa ujumla inaweza kuwa nzuri tu kwa kuku wa aina yoyote endapo mfugaji atafuga kitaalam na kufuata vizuri kanuni zote za ufugaji.

No comments:

Post a Comment